Kiongozi wa upinzani Venezuela Maria Corina Machado arejea nchini baada ya miezi kadhaa uhamishoni
Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela, Maria Corina Machado, amerejea nchini humo baada ya kukaa nje ya nchi kwa zaidi ya miezi 10, wakati hali ya kisiasa ikiendelea kuwa na mvutano.
“Nimerudi hapa, niko pamoja nanyi,” aliandika Machado kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili.
Edmundo Gonzalez Urrutia, aliyewahi kugombea urais nchini Venezuela na ambaye ni mshirika wa Machado, pia alithibitisha taarifa hizo dakika chache baadaye.
“Nina furaha kuwajulisha kwamba kiongozi wetu, mpendwa wangu Maria Corina, yuko nchini Venezuela,” aliandika.
Aliongeza kuwa hivi karibuni atajiunga na Machado nchini humo ili kuongoza juhudi za kuifikisha nchi hiyo kwenye “uhuru”.
Mmoja wa washauri wa Machado alisema mwezi Septemba kuwa alikuwa amejaribu kurejea Venezuela mara saba katika wiki chache zilizotangulia, lakini alizuiwa kuingia nchini kila mara.
Bado haijafahamika Machado anapanga kufanya nini baada ya kurejea. Hata hivyo, amewahi kusema kuwa atawania tena urais iwapo uchaguzi utafanyika.
Katika taarifa iliyotolewa kwa Margaret Brennan wa CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, msemaji wa Machado alielezea kurejea kwake kuwa “hatua muhimu kuelekea mpito wa kidemokrasia na kufanyika kwa uchaguzi huru, wa haki na unaoweza kuthibitishwa katika siku za usoni”.
Soma Pia: