Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Matokeo ya awali ya uchaguzi Israel hayaonyeshi mshindi wa wazi

Netanyahu na Eisenkot wote wadai ushindi baada ya uchaguzi kukosa mshindi wa wazi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Likud ya Netanyahu yaongoza kwa asilimia 25 ya kura zilizohesabiwa

    Tume Kuu ya Uchaguzi ya Israel imesema zaidi ya kura milioni 1.6 zimehesabiwa katika uchaguzi wa bunge nchini humo.

    Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizosasishwa saa 4:47 asubuhi kwa saa za nchini Israel, chama cha Likud kinachoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kinaongoza kwa kupata asilimia 24.22 ya kura zilizohesabiwa.

    Chama cha Yashar kinachoongozwa na Gadi Eisenkot kinafuata, kikiwa na asilimia 41.15 ya kura, huku Muungano wa Pamoja (Joint List), unaojumuisha Waarabu na Wayahudi, ukiwa nafasi ya tatu kwa asilimia 28.8.

    Chama cha Yisrael Beitenu kinachoongozwa na Naftali Bennett kinafuata kwa asilimia 22.8 ya kura.

  2. Abiria wa meli ya kifahari ya kitalii wamekwama nchini Kambodia kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta

    Abiria wa meli ya kifahari iliyokuwa ikizunguka dunia wamekwama nchini Cambodia baada ya kampuni inayoendesha meli hiyo kusitisha safari kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta.

    Kampuni ya Marekani inayomiliki meli ya Villa Vie Odyssey imesema inashirikiana na abiria kupanga namna ya kushuka melini na kupata makazi ya muda.

    Haijafahamika idadi kamili ya abiria waliokuwa melini, lakini meli hiyo yenye urefu wa karibu mita 200 ina uwezo wa kubeba hadi abiria 650. Ilianza safari yake kutoka Belfast, Ireland Kaskazini, mwezi Oktoba 2024, ikiwa na mpango wa kuzunguka dunia.

    Bei ya mafuta imepanda kwa kiasi kikubwa tangu kuanza kwa vita vya Iran mapema mwaka huu. Kampuni hiyo imesema gharama ya mafuta kwa kila chumba cha abiria kwa mwezi katika baadhi ya maeneo ya Asia imeongezeka kutoka dola 1,800 hadi dola 8,000.

    Kampuni hiyo imesema ilichukua hatua za kupunguza matumizi ya mafuta, zikiwemo kupunguza kasi ya meli na kuongeza muda wa kusimama bandarini. Hata hivyo, hatua hizo hazikutosha kukabiliana na ongezeko kubwa la gharama.

    Kampuni hiyo imesema haiwezekani kuwabebesha abiria gharama zote za ongezeko hilo.

    Imeongeza kuwa itatumia siku 60 zijazo kurekebisha shughuli zake na kutafuta mtaji zaidi, ingawa hakuna uhakika wa matokeo ya mchakato huo.

    Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni hiyo, safari hiyo ilipangwa kudumu miaka mitatu na nusu na kutembelea karibu nchi 150.

    Meli hiyo ilikuwa imezunguka dunia kwa zaidi ya siku 750 ilipotangaza kusitisha safari yake Jumanne, na kuwaacha abiria nchini Cambodia.

    Shirika la habari la Bloomberg, likimnukuu mwanzilishi wa kampuni hiyo, limeripoti kuwa takribani abiria 200 walikuwa melini walipoambiwa washuke nchini Cambodia.

    Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni hiyo, meli ya Villa Vie Odyssey ina baa na mikahawa kadhaa, eneo la kuogelea na uwanja wa mchezo wa pickleball.

  3. Cameroon yasitisha shughuli za chama cha upinzani baada ya ghasia za uchaguzi

    Waziri wa Utawala wa Maeneo nchini Cameroon amesitisha kwa miezi mitatu shughuli za chama cha kiongozi wa upinzani Issa Tchiroma Bakary, akikituhumu kwa utovu wa nidhamu kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa urais uliokuwa na utata mwaka jana.

    Katika agizo lililotolewa leo, Waziri Paul Atanga Nji amekituhumu chama cha Cameroon National Salvation Front (CNSF) kwa kuchochea uasi na ghasia, kutishia uadilifu wa eneo la nchi, umoja wa kitaifa na mamlaka ya kujitawala, pamoja na kuvuruga amani na usalama wa umma.

    “Shughuli zote za chama cha kisiasa kinachojulikana kama Cameroon National Salvation Front (CNSF) zimepigwa marufuku na zitaendelea kuwa marufuku katika eneo lote la nchi katika kipindi cha kusimamishwa kwake,” amesema Nji.

    Uamuzi huo umefikiwa kabla ya uchaguzi muhimu wa serikali za mitaa na bunge unaotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka ujao. Hatua hiyo imeibua dhana kwamba huenda lengo ni kukizuia chama cha Tchiroma kushiriki katika chaguzi hizo mbili.

    Hata hivyo, kiongozi huyo wa upinzani, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Gambia, alikuwa amesema awali kuwa chama chake hakitashiriki uchaguzi huo. Alisema mazingira yanayohitajika kwa uchaguzi wa kidemokrasia, uwazi na amani hayajatimizwa.

    Katika taarifa iliyotolewa mwezi Februari, chama hicho kilisema kushiriki katika mchakato huo kungekuwa sawa na kuhalalisha utawala ambao, kwa mtazamo wake, ulishindwa kwenye uchaguzi, na kuunga mkono uchaguzi ambao matokeo yake tayari yameamuliwa.

    BBC imewasiliana na msemaji wa Tchiroma Bakary kutaka maoni yake kuhusu kusimamishwa kwa shughuli za chama hicho.

    Tchiroma alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 2025, lakini akajitangaza kuwa mshindi halali dhidi ya aliyekuwa bosi wake, Paul Biya. Alidai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na ukiukaji mkubwa wa taratibu na kutoa wito wa maandamano ili kutetea kile alichokiita ushindi wake.

    Katika baadhi ya miji nchini humo, maandamano yaligeuka kuwa ghasia zilizosababisha uharibifu wa majengo ya umma na miundombinu mingine.

    Tume ya Haki za Binadamu ya Cameroon ilisema watu 14 waliuawa katika mapigano kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji waliopinga kile walichokitaja kuwa udanganyifu wa uchaguzi. Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu, zaidi ya watu 1,200 walikamatwa na kuwekwa kizuizini.

    Mapema mwezi huu, mahakama katika mji mkuu wa Yaoundé iliwahukumu zaidi ya watu 60 waliokamatwa kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi. Baadhi yao walifungwa jela kwa kati ya miezi sita na 15.

    Soma Pia:

  4. Tetesi za soka Jumatano: Liverpool yamfukuzia beki wa Stuttgart Jeltsch

    Liverpool, Barcelona na Real Madrid ni miongoni mwa klabu kubwa za Ulaya zinazomfuatilia beki wa kati wa Stuttgart, Finn Jeltsch, mwenye umri wa miaka 20 na raia wa Ujerumani.

    Chelsea imeelekeza nguvu zake katika kumsajili kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, mwenye umri wa miaka 23, baada ya uhamisho wake kushindikana dirisha lililopita. Liverpool pia imemjumuisha mchezaji huyo wa England katika orodha ya wanaowindwa.

    Chelsea, Manchester City, Arsenal, Tottenham na Newcastle zimekuwa zikituma maskauti kumfuatilia mshambuliaji wa Club Brugge, Nicolo Tresoldi, ambaye amewahi kuiwakilisha Ujerumani katika ngazi za vijana. Hata hivyo, Club Brugge haiko tayari kumuuza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 katika dirisha la Januari.

    Manchester United ilipanga kumtimua kocha Michael Carrick wiki hii, lakini imeshindwa kukubaliana kuhusu atakayechukua nafasi yake.

    United italazimika kulipa Newcastle takribani pauni milioni 3 kama fidia iwapo itaamua kumteua Eddie Howe kuwa mrithi wa Carrick.

    Brighton haina wasiwasi wa kumpoteza kiungo wa Paraguay, Diego Gomez, mwenye umri wa miaka 23, licha ya kuvutiwa naye kwa AC Milan na Atletico Madrid.

    Kocha Pierre Sage anaendelea kukabiliwa na shinikizo kubwa, na anaweza kutimuliwa iwapo Crystal Palace itafungwa na Tottenham Jumamosi.

    Liverpool itafuatilia uwezekano wa kumsajili winga wa Valencia, David Otorbi, mwezi Januari iwapo klabu hiyo ya La Liga itaongeza kipengele cha kuvunja mkataba wake kutoka pauni milioni 30 hadi milioni 50. Otorbi ana umri wa miaka 19 na ni raia wa Hispania.

    Juventus imemweka mshambuliaji wa Monaco, Folarin Balogun, kuwa kipaumbele chake katika dirisha la usajili la Januari. Mshambuliaji huyo wa Marekani mwenye umri wa miaka 25 aliwahi kukaribia kujiunga na Everton siku ya mwisho ya dirisha la usajili, lakini uhamisho huo ukakwama.

    Soma pia:

  5. Flávio Bolsonaro afika Marekani baada ya Brazil kufuta hati zake za usafiri

    Mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi wa urais wa Brazil, Flávio Bolsonaro, amewasili Marekani saa chache baada ya mamlaka za Brazil kufuta hati zake za kusafiria, vyanzo vimeiambia BBC.

    Bolsonaro, mwanasiasa wa mrengo wa kulia, aliondoka Brazil baada ya Mahakama ya Juu kuamuru akabidhi hati zake za kusafiria, wakati uchunguzi kuhusu madai ya utakatishaji fedha ukiendelea. Hata hivyo, hajafunguliwa mashtaka na amekanusha madai hayo.

    Hati zake zilifutwa Jumanne baada ya kushindwa kuzikabidhi kwa mamlaka ndani ya muda uliowekwa, hatua iliyozua uvumi kuhusu uwezekano wa kuondoka nchini humo.

    Vyanzo vilivyozungumza na BBC Brasil na BBC Mundo vimesema Flávio alikutana na mdogo wake, Eduardo, katika jimbo la Florida, Marekani. Hata hivyo, haijulikani njia aliyotumia kusafiri kutoka Brazil hadi Marekani.

    Hakuna kati ya ndugu hao aliyeweza kupatikana moja kwa moja ili kutoa maoni yake.

    Kuwasili kwake kunaripotiwa saa chache baada ya afisa mwandamizi wa Marekani kuthibitisha kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo itatoa visa kwa Bolsonaro na familia yake na kuwaruhusu kuingia Marekani.

    BBC imewasiliana na Ikulu ya Marekani, Wizara ya Mambo ya Nje na balozi za nchi hizo mbili kupata maelezo zaidi.

    Siku ya Jumatatu, Mahakama ya Juu ya Brazil iliamuru Bolsonaro akabidhi hati zake za kusafiria kwa polisi ndani ya saa 24, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa madai ya utakatishaji fedha.

    Bolsonaro pia alikuwa akichunguzwa kuhusu madai ya ufisadi katika ufadhili wa filamu inayomhusu baba yake, rais wa zamani Jair Bolsonaro. Jair alitiwa hatiani kwa kupanga njama ya mapinduzi na kwa sasa yuko chini ya kifungo cha nyumbani.

    Uchunguzi mwingine unahusu madai ya uhusiano wake na wakili wa Brazil anayetuhumiwa kutakatisha zaidi ya dola bilioni moja kupitia mpango wa ulaghai.

    Flávio amekanusha kufanya biashara na wakili huyo na kueleza kuwa kunyang’anywa hati zake za kusafiria ni jaribio la kumtisha.

    Bado haijulikani ni nani aliyesafiri naye kwenda Marekani, au iwapo anakusudia kubaki nchini humo na kuishi huko.

    Soma Pia:

  6. Matokeo ya awali ya uchaguzi Israel hayaonyeshi mshindi wa wazi

    Matokeo ya awali ya kura za maoni zilizofanywa baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura nchini Israel yanaashiria kuwa hakuna mshindi wa wazi katika uchaguzi mkuu unaotajwa kuwa muhimu kwa mustakabali wa nchi hiyo.

    Waziri Mkuu wa zamani Benjamin Netanyahu wala aliyekuwa mkuu wa jeshi, Gadi Eisenkot, hawaonekani kuwa na uhakika wa kupata viti vya kutosha kuunda serikali kwa wingi wa wabunge.

    Taarifa za vituo viwili vya utangazaji nchini Israel zinaonyesha kuwa chama cha Yashar cha Eisenkot na vyama vingine vitatu vya upinzani vinavyounda muungano wa kisiasa unaoitwa Change Bloc vinatarajiwa kupata viti 51 kati ya 120 katika bunge la Israel, Knesset. Idadi hiyo ni sawa na inayotarajiwa kupatikana na chama cha Likud cha Netanyahu pamoja na washirika wake wa mrengo mkali wa kulia na vyama vya Wayahudi wa Kiorthodoksi kali.

    Hata hivyo, kura ya maoni ya kituo kingine cha utangazaji inampa Netanyahu uongozi wa viti vitatu.

    Mwelekeo wa kuundwa kwa serikali unaweza kutegemea kwa kiasi kikubwa nafasi ya vyama viwili vya Waarabu, ambavyo vinatarajiwa kupata jumla ya viti 18 au 19, idadi ambayo ingekuwa rekodi.

    Ushiriki wa wapiga kura Jumanne ulikuwa mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.

    Tume Kuu ya Uchaguzi imesema kuwa idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa asilimia 77.7 wakati vituo vilipofungwa saa nne usiku kwa saa za Israel. Huo ndio ulikuwa kiwango cha juu zaidi kufikia muda huo tangu mwaka 1999.

    Matokeo rasmi yanatarajiwa kuanza kutangazwa usiku kucha. Hata hivyo, kura takribani 600,000 zilizopigwa na wapiga kura wasiokuwepo katika maeneo yao, wengi wao wakiwa wanajeshi, hazitakuwa zimehesabiwa kikamilifu hadi Alhamisi. Kura hizo zinakadiriwa kuwa takribani asilimia 10 ya kura zote.

    Baada ya matokeo ya mwisho kuthibitishwa na rais wa Israel kufanya mashauriano na makundi yote ya kisiasa, atamwalika kiongozi wa chama anayeona ana nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa kuunda muungano wa serikali.

    Mchakato huo unaweza kuchukua wiki kadhaa. Iwapo juhudi za kuunda serikali zitashindikana, uchaguzi mwingine utalazimika kufanyika.

    Eisenkot amesema wameandika historia na kuahidi kuhakikisha kuwa uamuzi wa wananchi unatafsiriwa katika kuundwa kwa serikali ya Kizayuni ambayo itakuwa imara na yenye manufaa kwa raia wote wa Israel.

    Hata hivyo, katika makao makuu ya chama cha Likud cha Netanyahu mjini Jerusalem, hakukuwa na dalili za kukubali kushindwa.

    Kura za maoni zinaonyesha kuwa Likud bado inaweza kuwa chama chenye viti vingi zaidi bungeni.

    Soma Pia:

  7. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 28/10/2026.