Je, vinasaba vinaamua hatima ya binadamu?

Mwanamke akipokea matibabu ya tiba ya sindano za Kichina (acupuncture) kwa ajili ya kupunguza mikunjo na dalili za kuzeeka.

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, بتول حبيبه
    • Nafasi, بي بي سي عربي
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Unaposikia kuhusu sayansi ya maisha marefu, huenda jambo la kwanza linalokujia akilini ni kuishi muda mrefu zaidi. Lakini dhana hii ina maana pana zaidi; lengo si kuongeza tu idadi ya miaka ya kuishi, bali pia kuishi miaka hiyo ukiwa na afya bora na nguvu zaidi.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la mijadala kuhusu sayansi ya maisha marefu na kupambana na kuzeeka, fani inayolenga kuongeza miaka yenye afya, badala ya kuongeza tu miaka ya maisha.

Daktari bingwa wa tiba ya familia na magonjwa sugu, Dk Bayan Abu Al-Sheikh, anasema tatizo si kufikisha umri fulani, bali ni kupoteza uwezo wa kutembea na kujitegemea, pamoja na kuanza kupata magonjwa sugu kadiri umri unavyoongezeka.

Kwa hiyo, kwa mujibu wa Abu Al-Sheikh, sayansi ya maisha marefu inalenga kuwasaidia watu kufikia umri mkubwa huku wakidumisha uwezo wa kutembea, kujitegemea na kufurahia maisha.

"Namba hazidanganyi"

Katika mahojiano na BBC News Arabic, daktari huyo anaeleza kuwa hakuna fomula ya kimiujiza ya kuongeza maisha yenye afya na kupambana na kuzeeka. Badala yake, yote huanza na misingi ya maisha yenye afya, kama vile kupata usingizi mzuri, kula lishe bora na kufanya mazoezi.

Anaamini kuwa usingizi mzuri ni miongoni mwa mambo muhimu yanayohusishwa na maisha marefu na yenye afya. Anataja uwezekano wa kutumia vifaa kama WHOOP na Oura kufuatilia ubora wa usingizi na hatua zake, hasa usingizi mzito.

Anaongeza kuwa kutathmini iwapo mtu anazeeka kwa kasi kuliko kawaida hutegemea viashiria muhimu vya afya na vipimo vya maabara, huku uchambuzi wa DNA ukiweza kutoa picha kuhusu umri wa kibaiolojia wa mtu.

Watu wawili wanaweza kuwa na umri sawa, lakini mmoja akawa na viashiria bora vya afya na umri mdogo zaidi wa kibaiolojia kuliko mwingine.

Mchezaji wa soka wa Ureno, Cristiano Ronaldo, ni miongoni mwa watu mashuhuri ambao wamezungumza hadharani kuhusu maisha marefu na afya. Katika mahojiano ya podcast na Will Ahmad, mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Whoop, alizungumzia tabia na falsafa yake kuhusu afya, nidhamu na kudumisha utimamu wa mwili kadiri anavyozeeka.

Katika mahojiano hayo, alisisitiza umuhimu wa kupata usingizi wa kawaida pamoja na kufanya mazoezi mara kwa mara, akisema kuwekeza katika afya kunaonekana katika ubora wa maisha.

Picha ya Cristiano Ronaldo ikionekana kwa nyuma, huku uso wake ukionekana kwenye kioo kilicho mbele yake, akiwa ananyanyua chuma gym na amevaa kifaa cha WHOOP mkononi kinachopima ubora wa usingizi na viashiria vya mwili.

Chanzo cha picha, youtube

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa mujibu wa Abu Al-Sheikh, vipimo muhimu vinajumuisha kupima kiwango cha misuli, asilimia ya mafuta mwilini na msongamano wa mifupa, pamoja na kutathmini afya ya moyo na mapafu, kiwango cha ubadilishanaji wa nishati mwilini, hali ya ngozi na matumizi ya oksijeni, yanayojulikana kama "VO2".

Kwa mujibu wa matokeo hayo, daktari anaweza kuandaa mpango wa kuboresha viashiria vya afya kupitia lishe, mazoezi au usingizi. Mpango huo unaweza pia kujumuisha baadhi ya vitamini au virutubisho inapohitajika na chini ya usimamizi wa daktari.

Abu Al-Sheikh anasema kufuata mpango huo kwa muda huonekana katika matokeo ya vipimo na viashiria vya afya, akiongeza: "Namba hazidanganyi."

Pia anasisitiza kwamba mtu mwenyewe ana jukumu la msingi katika afya yake. Anaeleza kuwa jukumu la daktari ni kutambua matatizo na kuandaa mpango unaofaa, lakini kufuata ratiba ya usingizi, lishe, mazoezi na ufuatiliaji wa afya ni jukumu la mtu binafsi.

Kwa upande wake, Ghaliya, ambaye alianza kufuata mpango wa kuongeza miaka yenye afya chini ya usimamizi wa daktari, anasema hamu yake katika eneo hili haitokani na hofu ya kuzeeka, bali ni kutaka kufikia uzee akiwa na afya bora.

Anaongeza kuwa anajali kuonekana mwenye umri mdogo kuliko umri wake halisi, lakini jambo muhimu zaidi kwake ni kuzeeka akiwa na afya njema na bila magonjwa au maumivu.

Anaiambia BBC kwamba ameanza kufanya vipimo na kufuata mpango wa lishe, lakini haoni kama ni mpango wa muda mfupi, bali ni mtindo wa maisha.

Pia amekuwa makini zaidi kuhusu ubora wa chakula anachokula na amerudi kufanya mazoezi gym. Anasema sasa analala vizuri zaidi baada ya kuanza kutumia vitamini na virutubisho alivyopendekezewa na daktari.

Sayansi au biashara?

Abu Al-Sheikh, ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya maisha marefu yenye afya na kupambana na kuzeeka, anasema baadhi ya nchi zimeanza kuweka kanuni katika eneo hili kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za kuongeza miaka yenye afya ndani ya mifumo ya kitabibu iliyo wazi zaidi.

UAE ni miongoni mwa nchi za kwanza katika eneo hilo kuchukua hatua za kudhibiti utaalamu huu, kupitia kuanzisha programu za kitaaluma na kliniki zinazobobea katika maisha marefu na kuzeeka kwa afya.

Programu hizo hazihusishi madaktari pekee, bali pia wafamasia, wauguzi, wataalamu wa tiba ya viungo, wataalamu wa lishe, wakufunzi wa mazoezi na wataalamu wengine wa afya.

Abu Al-Sheikh anakosoa namna watu wasio wataalamu wanavyozungumzia eneo hili kwenye mitandao ya kijamii, akisema mijadala kuhusu mipango ya "maisha marefu yenye afya" mara nyingi hugeuka kuwa matangazo ya bidhaa fulani.

Anasema mpaka kati ya sayansi na "mtindo unaovuma" huonekana pale ambapo uuzaji wa kibiashara wa bidhaa maalumu unapoanza.

Wageni wakijaribu bidhaa ya “kupambana na kuzeeka” katika jiji la Cologne, magharibi mwa Ujerumani, Aprili 17, 2026.

Chanzo cha picha, Getty Images

Wakati huo huo, Abu Al-Sheikh anahusisha kuenea kwa dhana za maisha marefu na kupambana na kuzeeka na kuongezeka kwa uelewa wa afya pamoja na mijadala mingi kuhusu mada hizo kwenye mitandao ya kijamii.

Anasema dhana ya ustawi imebadilika duniani. Haitegemei tena fedha na mali pekee; sasa kuwekeza katika afya kumekuwa pia sehemu ya ustawi wa maisha.

Kwa mujibu wake, kuongezeka kwa viwango vya unene kupita kiasi na magonjwa sugu pia kumewafanya watu kuvutiwa zaidi na kinga.

Anaeleza kuwa taarifa za afya zinawafikia watu kwa kasi zaidi kuliko zamani, lakini kasi ya kusambaa kwa taarifa haimaanishi kwamba taarifa hizo ni sahihi, "na hapo ndipo tatizo linapoanzia", jambo linalofanya udhibiti wa mchakato huo kuwa muhimu.

Miongoni mwa maneno yanayotumika sana katika ulimwengu wa maisha marefu yenye afya kwa sasa ni peptidi (peptides), ambazo ni minyororo ya amino asidi. Abu Al-Sheikh anasema kazi zake hutofautiana kulingana na muundo wake.

Anaeleza kuwa baadhi ya dawa za kisasa ziko katika kundi hili au hufanya kazi kupitia mifumo inayohusiana nalo, ikiwemo baadhi ya dawa zinazotumika kutibu kisukari na kupunguza uzito.

Je, vinasaba ndivyo vinaamua hatima yetu?

Katika miongo miwili iliyopita, tafiti nyingi zimejikita katika genetics na epigenetics.

Abu Al-Sheikh anaeleza kuwa, kuwa na jeni inayohusishwa na ugonjwa fulani hakumaanishi moja kwa moja kwamba mtu ataugua ugonjwa huo, kwa sababu mambo kama mazingira, mtindo wa maisha, lishe, usingizi na mazoezi yanaweza kuathiri namna vinasaba vinavyofanya kazi.

Hapo ndipo epigenetics inapohusika. Ni taaluma inayochunguza jinsi mazingira na mambo yanayomzunguka mtu yanavyoathiri utendaji wa vinasaba bila kubadilisha mfuatano wa DNA wenyewe.

Kwa hiyo, Abu Al-Sheikh anaamini kwamba kuwa na mwelekeo wa kinasaba wa kupata ugonjwa hakupaswi kuchukuliwa kama hukumu ya mwisho.

Kuhusu kuzeeka, anasema mtazamo wa kisayansi kuhusu suala hilo pia umebadilika. Hapo awali, kuzeeka kulionekana kama hatua ya kawaida ya kisaikolojia, lakini leo kuna mwelekeo wa kisayansi unaokichukulia kama hali ambayo michakato yake inaweza kuingiliwa, huku kukiwa na ongezeko la hamu ya kuchelewesha dalili za kudhoofika zinazohusishwa na kuzeeka.

Hata hivyo, Ghaliya anaamini kwamba kuzingatia sana kuongeza miaka yenye afya na kupambana na kuzeeka kunaweza wakati mwingine kuwa chanzo cha msongo wa kisaikolojia, hasa kwa watu wanaojishughulisha kupita kiasi na mwonekano wao na kujaribu kupambana na dalili za kuzeeka.

Lakini kwa wale wanaotaka tu kuzeeka kwa afya na kuishi miaka yao wakiwa na magonjwa na maumivu machache iwezekanavyo, hali ni tofauti.

Ghaliya anasema wazo hili halipaswi kuwa chanzo cha msongo wa mawazo, bali linapaswa kuwa msukumo wa kufuata mtindo wa maisha wenye afya ambao mtu anaweza kuudumisha kwa muda mrefu.