Vyakula 5 vya Kiafrika ambavyo sayansi inaviona kuwa bora kwa afya

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Kuanzia Moringa hadi Fonio, na ikijumuisha Baobab, Mtama, na Teff, vyakula kadhaa vya Kiafrika vinajulikana kwa utajiri wake wa virutubisho.

Baadhi yake hata huchukuliwa kuwa "vyakula bora zaidi" (superfoods) kutokana na wingi wa virutubisho vilivyomo na faida nyingi zinazotokana navyo.

Hebu tuvifahamu baadhi ya vyakula hivyo.

1- Moringa

Mara nyingi huitwa "mti wa miujiza" kwa sababu ya sifa zake nyingi zinazodaiwa kuwa na manufaa, moringa oleifera ni miongoni mwa mimea yenye virutubisho vingi hasa Vitamini A na C, protini, chuma, kalsiamu, potasiamu, magnesiamu, lipidi, wanga, na nyuzinyuzi hufanya chakula hiki kuwa chakula cha kuvutia sana kutoka kwa mtazamo wa lishe.

Moringa, asili yake ikiwa Afrika na Asia Kusini, inajulikana kwa kutoa ulinzi wa antioxidant kupitia virutubisho vyake. Hivyo husaidia kulinda seli kutokana na uharibifu unaosababishwa na molekuli zinazoitwa free radicals.

Ingawa majani yake ndiyo yenye thamani zaidi, kwa sifa zake za lishe, yanaweza kuliwa mabichi, kukaushwa, au kusagwa kuwa unga. Sehemu zingine za mti huu pia hutumiwa, ikiwa ni pamoja na mbegu, maua, mizizi, na magome yake.

Aidha, sifa hizi za kupambana na oksidesheni (antioxidant) husaidia kuimarisha utendaji wa ubongo, na hivyobasi kusaidia katika kupambana na shida ya kupoteza kumbukumbu (dementia) na ugonjwa wa Alzheimer.

Uchunguzi wa kimaabara unaonyesha hasa kuwa sehemu fulani za majani yake, matunda au mizizi yake zinaweza kuathiri michakato inayohusika na uvimbe mwilini.

Hili ni jambo muhimu sana, ikizingatiwa kuwa uvimbe unahusika katika kusababisha magonjwa mengi sugu, ikiwemo unene uliopitiliza na kisukari.

Baadhi ya tafiti pia zinaonyesha kwamba moringa inaweza kusaidia kudhibiti sukari kwenye damu. Utafiti uliofanywa kwenye majani yake, haswa, unaonyesha kwamba yanaweza kuchochea seli za kongosho, ambazo zina jukumu la kutoa insulini, homoni inayosaidia kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu.

Miongoni mwa faida zake, majaribio ya hivi karibuni pia yanaihusisha na sifa zake za kupambana na saratani, ambazo zinaweza kupambana na saratani ya ini, na pia dhidi ya mfadhaiko.

Kipengele kingine tofauti: moringa hukua haraka na hustahimili ukame kiasi, na kuifanya kuwa mmea unaofaa sana kwa maeneo fulani ya kitropiki na kame.

2- Nafaka ya njaa{fonio}

Fonio ina historia ya zaidi ya miaka 5,000 na hulimwa katika takriban nchi kumi za Afrika Magharibi, zikiwemo Guinea, Mali, Benin, Senegal, Burkina Faso, Togo na Niger.

Kwa sababu ya punje zake ndogo zinazofanana na mchanga—jambo linalofanya wakati mwingine iitwe "nafaka yenye punje ndogo"—fonio inajulikana sana kwa thamani yake ya lishe na urahisi wa kusagwa mwilini.

Haina gluteni na ina kiwango kikubwa cha madini ya chuma, magnesiamu, zinki, kalsiamu, pamoja na nyuzinyuzi. Miongoni mwa faida nyingine, husaidia kupambana na upungufu wa damu, kupunguza msongo wa mawazo, na kuimarisha kinga ya mwili.

Wataalamu wa lishe wanashauri kunywa maji mengi wakati wa kula zao hili ili kurahisisha mchakato wa usagaji na ufyonzwaji wa virutubisho mwilini.

3- Mbuyu

Mmea mwingine maarufu wa bara la Afrika ni mbuyu. Sio tu matunda yake, bali pia majani yake hutumika kama chakula.

Tunda la mbuyu linathaminiwa sana, hasa kwa ajili ya kutengeneza juisi. Ili kuitayarisha, sehemu ya ndani ya tunda (nyama yake) inaweza kulowekwa na kisha kuchujwa.

Maziwa au viungo vingine vinaweza kuongezwa kabla ya kunywa.

Linapendwa sana kutokana na ladha yake, lakini pia kwa faida zake za lishe. Kwa hakika, tunda la mbuyu lina kiwango kikubwa cha vioksidishaji (antioxidants) na nyuzinyuzi (fiber), pamoja na potasiamu na vitamini C; virutubisho hivi husaidia mtu kuhisi kushiba na vinaweza kusaidia katika kudhibiti uzito wa mwili.

Kwa upande mwingine, majani ya mbuyu hutumika katika mapishi katika nchi kadhaa za Afrika Magharibi, hasa Benin, Togo, na Ghana.

Hutumika kutengeneza "mchuzi wa majani ya mbuyu," mchuzi ambao huwa na hali ya kunata kidogo lakini unathaminiwa sana. Pia yanajulikana kwa kuwa na kiwango kikubwa cha kalsiamu, potasiamu, madini ya chuma, madini mengine, protini, pamoja na vitamini B na C, na provitamin A.

Hii husaidia kupambana na upungufu wa damu, kuimarisha kinga ya mwili, na kupambana na maambukizi.

4- Mtama

Mtama ni chanzo cha nyuzinyuzi, magnesiamu, na misombo mingi inayotokana na mimea; ni miongoni mwa nafaka zinazolimwa kwa wingi zaidi katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, na pia katika nchi za Ulaya—hasa Ufaransa—ambako uzalishaji wake unaongezeka.

Kwa asili hauna gluteni na una kiwango cha chini cha mafuta, hivyo unaweza kuliwa kwa namna mbalimbali: kupikwa kama wali, kusagwa kuwa unga, au kutumika katika mapishi mengi ya asili.

Una faida nyingi kiafya, huku tafiti nyingine zikionyesha kuwa una uwezo wa kupunguza uvimbe na kufanya kazi kama kioksidishaji (antioxidant).

5- Teff

Teff ni nafaka ya kale inayolimwa hasa nchini Ethiopia, na inajulikana kwa sifa zake za kipekee za lishe.

Kwanza, ina kiwango kikubwa cha kalsiamu ikilinganishwa na nafaka nyingine.

Aidha, kwa kuwa haina gluteni kiasili, pia ina wingi wa madini ya chuma, nyuzinyuzi, protini, madini muhimu, na magnesiamu.

Ni chakula kinachopendekezwa na wanariadha wengi.