Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani yatoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake wanaoishi Mashariki ya Kati
Marekani pia imeonya kuwa Iran na makundi yanayoiunga mkono yanaweza kulenga maslahi mengine ya Marekani nje ya nchi, ikiwemo kampuni na taasisi zinazohusishwa na Marekani.
Muhtasari
- Makundi ya haki za binadamu yataka uchunguzi wa haraka kuhusu kutekwa kwa mhariri wa Shirika la habari
- Israel yatishia kulipiza kisasi iwapo Uingereza itaiwekea vikwazo
- Iran yaonya nchi zinazoshirikiana na Marekani kuishambulia
- Afisa wa jeshi Niger adai mataifa ya kigeni kuhusika katika uasi
- Trump: Sitaki kufanya mazungumzo ya amani na Iran
- Rais wa Ukraine azionya ndege za abiria kutotumia anga ya Urusi
- Mhariri wa shirika la habari aliyedaiwa kutekwa nyara kenya apatikana
- Rais wa Zambia aapishwa kwa muhula wa pili huku mpinzani wake akiwa amekamatwa
- Tunachojua kufikia sasa kuhusu shambulio la Marekani katika harusi huko Sirik Iran?
- Ujerumani yaishutumu Urusi kwa shambulio la uwanja wake wa ndege Leipzig
- Jeshi la Jordan ladai "kuzuia na kuharibu makombora 10 kati ya 13" yaliyofyatuliwa na Iran
- Trump: Sijaribu kuileta Iran kwenye meza ya mazungumzo
- Ujerumani yaishutumu Urusi kwa shambulio la uwanja wake wa ndege Leipzig
- Iran yalipiza kisasi baada ya mashambulizi ya Marekani kuua watu wanne katika harusi
Moja kwa moja
Na Abdalla Seif Dzungu & Mariam Mjahid
Tshisekedi na Netanyahu kuimarisha ushirikiano wa usalama na uchumi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Félix Tshisekedi, na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi kati ya nchi zao.
Taarifa kutoka ofisi ya Rais Tshisekedi imesema alifanya mazungumzo pia na Rais wa Israel, Isaac Herzog, kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano katika sekta mbalimbali.
Katika mazungumzo yake na Netanyahu, viongozi hao walijadili masuala ya usalama, kijeshi, kilimo, miundombinu, nishati na teknolojia ya kisasa.
Ofisi ya Netanyahu imetoa video ikimuonyesha akiwa pamoja na Tshisekedi, akisema:
"Ni furaha kumkaribisha rafiki yetu mkubwa, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hapa Israel.
Karibu Jerusalem."
Ziara ya Rais Tshisekedi nchini Israel ilianza Jumatatu.
Marekani kuondoa wanajeshi 200 kutoka Nigeria
Marekani inapanga kuwaondoa karibu wanajeshi 200 kutoka Nigeria, miezi michache tu baada ya kupelekwa nchini humo kusaidia kukabiliana na hali ya usalama inayozidi kuwa mbaya.
Wanajeshi hao wanatarajiwa kuondoka Nigeria ifikapo mwisho wa mwezi Septemba.
Licha ya uamuzi huo wa ghafla, jeshi la Nigeria limesema hatua hiyo haimaanishi kuwa ushirikiano wake na Washington umekatika au kudhoofika.
Wakati wa uwepo wao nchini humo, wanajeshi wa Marekani walitoa mafunzo kwa jeshi la Nigeria, kushirikiana taarifa za kijasusi na kusaidia katika operesheni iliyomuua kiongozi mkuu wa kundi la Islamic State.
Jeshi la Nigeria limesisitiza kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili bado ni imara na haujabadilika.
Marekani yatoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake wanaoishi Mashariki ya kati
Marekani imewataka raia wake wanaoishi au kusafiri katika nchi za Mashariki ya Kati kuwa waangalifu zaidi kutokana na hofu ya mashambulizi ya Iran na kuongezeka kwa vurugu katika eneo hilo.
Ubalozi wa Marekani Abu Dhabi na Dubai umewaonya raia wake kujiandaa kwa uwezekano wa kufutwa kwa safari za ndege, kufungwa kwa anga na usumbufu mwingine wa usafiri.
Marekani pia imeonya kuwa Iran na makundi yanayoiunga mkono yanaweza kulenga maslahi mengine ya Marekani nje ya nchi, ikiwemo kampuni na taasisi zinazohusishwa na Marekani.
Pia unaweza kusoma:
Makundi ya haki za binadamu yataka uchunguzi wa haraka kuhusu kutekwa kwa mhariri wa Shirika la habari
Baraza la Vyombo vya Habari Kenya MCK na Mashirika ya haki za binadamu yamelaani kutekwa kwa mhariri wa gazeti la Standard, Alex Kiprotich, na kutaka uchunguzi wa haraka kubaini kilichotokea na kuwawajibisha waliohusika.
Amnesty International Kenya imesema tukio hilo linazua wasiwasi kuhusu uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari, ikitaka uchunguzi huru na wa wazi.
Vile vile, Tume ya Haki za Binadamu Kenya KHRC imetaka waliohusika, wakiwemo makamanda iwapo maafisa wa usalama watahusishwa, wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
"KHRC inasisitiza kuwa maafisa waliohusika, wakiwemo makamanda wao, lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani bila kuchelewa," ilisema.
Wakati huo huo, vyama vya kisiasa vya KANU na ODM pia vimelaani tukio hilo na kutaka uchunguzi ufanyike.
Mhariri huyo ameachiliwa, lakini aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria Kenya, Faith Odhiambo, amesema kutekwa kwake ni shambulio kubwa dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na utawala wa sheria.
"Ingawa tunafarijika kwamba ameachiliwa, kutekwa kwake bado ni shambulio kubwa dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari, utu wa binadamu, utawala wa sheria na haki ya kila Mkenya kuishi bila hofu," amesema.
Israel yatishia kulipiza kisasi iwapo Uingereza itaiwekea vikwazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar ameonya kuwa Israel itachukua hatua dhidi ya Uingereza iwapo London itaweka vikwazo kwa Israel kutokana na upanuzi wa makazi ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi.
Gideon Saar amesema: Ikiwa Uingereza itachukua hatua dhidi ya Israel, Israel italipiza kisasi.
Aidha, ameonya kuwa Uingereza itakuwa inafanya kosa kubwa iwapo itaweka vikwazo dhidi ya Israel.
Onyo hilo linakuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Ed Miliband kusema serikali itapitia upya sera yake kuhusu Israel.
Miliband amesema Uingereza itachunguza hatua za kuzuia kampuni zake kufadhili, kujenga au kutangaza makazi mapya katika Ukingo wa Magharibi.
Mwezi uliopita, Israel ilitangaza zabuni za kujenga takriban nyumba 1,200 katika eneo la E1, mpango ambao Miliband amesema ni kinyume cha sheria za kimataifa na unatishia uwezekano wa kuanzishwa kwa taifa la Palestina.
Iran yaonya nchi zinazoshirikiana na Marekani kuishambulia
Makao Makuu ya Khatam al Anbiya nchini Iran yameonya nchi za eneo hilo zinazoshirikiana na Marekani katika mashambulizi dhidi ya Iran kuwa zitakabiliwa na madhara makubwa.
Iran imesema ilijibu mashambulizi ya Marekani kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya vituo vya Marekani nchini Jordan, Bahrain na Erbil, Iraq.
Tehran pia imeonya nchi zinazohifadhi wanajeshi wa Marekani kwamba zitashambuliwa iwapo zitaendelea kuunga mkono operesheni za Marekani.
Iran pia imedai kuwa mashambulizi ya Marekani yaliwaua raia wasiopungua watano, akiwemo mtoto, wakati wa sherehe ya harusi kusini mwa nchi. Zaidi ya watu 60 wameripotiwa kujeruhiwa.
Afisa wa jeshi Niger adai mataifa ya kigeni kuhusika katika uasi
Afisa wa jeshi nchini Niger, Roger Gabriel, amedai kuwa mataifa ya kigeni yalihusika katika uasi wa kijeshi uliotokea katika kambi ya kijeshi ya 101 mjini Niamey tarehe 29 Agosti.
Amesema alipokea simu na ujumbe kutoka ndani na nje ya Niger, ukidai kuwa kulikuwa na uingiliaji wa kigeni uliowasaidia wanajeshi waliohusika katika uasi huo.
Afisa huyo amedai kuwa baadhi ya maafisa wa Chad na watu waliokuwa na uhusiano na rais wa zamani wa Niger, Mohamed Bazoum, walitaja uwezekano wa msaada wa kijeshi kutoka nje, ukiwemo vikosi maalum.
Hata hivyo, madai hayo hayajathibitishwa kwa ushahidi huru. Mamlaka za Niger zimesema hali imedhibitiwa.
Haya yanajiri baada ya Urusi kusema vikosi vyake vya Africa Corps vilisaidia vikosi vya Niger kukabiliana na jaribio la mapinduzi katika mji mkuu Niamey Jumamosi.
Trump: Sitaki kufanya mazungumzo ya amani na Iran
Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha ripoti ya ABC News kwamba utawala wake unajaribu kuishinikiza Iran kuingia katika mazungumzo.
Katika ujumbe kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema hana nia ya kufanya makubaliano na Tehran.
Amesema angependelea hali ya sasa, huku Marekani ikiwa karibu kudhibiti kikamilifu Mlango wa Hormuz na uchumi wa Iran ukiendelea kudorora.
Trump pia ametoa wito kwa wananchi wa Iran kujiinua dhidi ya serikali yao.
Kauli hiyo imekuja saa chache baada ya Trump kusema mashambulizi mapya ya Marekani karibu na Mlango wa Hormuz yalikuwa yanahalalika.
Ameonya kuwa Marekani itatekeleza mashambulizi makali zaidi iwapo Iran italipiza kisasi.
Iran imesema mashambulizi hayo yaliwalenga raia waliokuwa kwenye sherehe ya harusi katika kijiji cha Kohstak Sirik.
Kwa mujibu wa Iran, watu wasiopungua watano, akiwemo mtoto mmoja, wameuawa na zaidi ya watu 60 wamejeruhiwa.
Rais wa Ukraine azionya ndege za abiria kutotumia anga ya Urusi
Rais wa Ukraine ameyaambia mashirika ya ndege kwamba anga ya Urusi "itafungwa kikamilifu" huku nchi yake ikizidisha mashambulizi yake ya ndege zisizo na rubani.
"Tunataka kuionya kila ndege inayotumia anga ya Urusi, kila bima, kila mtu ambaye bado anatumia viwanja vya ndege muhimu vya Urusi: anga ya Urusi inazidi kuwa hatari," Volodymyr Zelensky anasema.
Mashirika mengi ya ndege ya kibiashara ya Magharibi hayaruki juu ya Urusi kutokana na uvamizi unaoendelea wa Urusi dhidi ya Ukraine, lakini mashirika ya ndege katika nchi kama vile China yanafanya hivyo.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alijibu kwa kusema kwamba maoni ya Zelensky yalikuwa sawa na "tamko la ugaidi", huku akiongeza kwamba Urusi itaendelea na mashambulizi yake yanayoongezeka dhidi ya Ukraine.
Akielezea hatari kubwa ya anga, Zelensky amesema: "Ukraine haitishii usafiri wa anga wa kiraia - hakuna ndege hata moja ya kiraia.
"Kutakuwa na ndege zisizo na rubani angani mwa Urusi kwa kiwango ambacho kinapaswa kuzingatiwa," alisema katika hotuba yake ya video ya usiku Jumanne.
Zelensky ameisema kwamba "vita vilivyoanzishwa na Urusi vinafunga anga zake".
Alielekeza onyo hilo kwa mashirika ya ndege yanayoendelea kuendesha safari za ndege hadi viwanja vya ndege vya Urusi, haswa katika miji mikubwa kama St Petersburg na Moscow.
Ukraine imelenga vituo vya nishati ndani kabisa ya eneo la Urusi pamoja na wauzaji wakubwa.
Kampuni ya ushauri wa hatari ya anga ya Osprey Flight Solutions ilisema katika tahadhari kwa wateja kwamba ingawa mashambulizi mengi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Ukraine yana uwezekano wa kutokea ndani ya kilomita 300 (maili 186) kutoka mpakani, mashambulizi ya kila siku ndani kabisa mwa Urusi yalikuwa karibu yaendelee mwaka huu.
Mhariri wa shirika la habari aliyedaiwa kutekwa nyara kenya apatikana
Mhariri wa shirika la habari la Standard Group, nchini Kenya Alex Kiprotich, ambaye inasemekana alitekwa nyara kando ya barabara ya Gilgil–Nakuru Jumanne usiku, alipatikana salama kwenye kichaka katika eneo la Masinga, Kaunti ya Machakos.
Mashahidi wanasema Kiprotich alionekana kutetemeka huku akiwa amejeruhiwa alipopatikana Jumatano asubuhi, saa chache baada ya tukio hilo kuripotiwa.
Alipatikana kilomita 200 kutoka mahali aliporipotiwa kutekwa nyara.
Wenzake na familia yake wanasema walipokea simu kutoka kwa nambari , walipopokea, wakamkuta Kiprotich kwenye simu.
Walikuwa wakimtafuta usiku kucha. Kiprotich alipelekwa hospitalini kwa uchunguzi.
Polisi wanasema waliarifiwa kuhusu ugunduzi huo na walikuwa wakichunguza mazingira. Sababu ya kutekwa nyara haijajulikana.
Rais wa Zambia aapishwa kwa muhula wa pili huku mpinzani wake akiwa amekamatwa
Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ameapishwa kwa muhula wa pili wa miaka mitano kufuatia uchaguzi uliogubikwa na utata na kukamatwa kwa mpinzani wake mkuu kwa tuhuma za uhaini.
Hichilema, ambaye anasifiwa kwa kuleta utulivu wa kiuchumi, alipata ushindi wa kishindo mnamo tarehe 13 Agosti kwa kujipatia asilimia 60 ya kura, kulingana na matokeo rasmi.
Mpinzani wake wa karibu, Brian Mundubile, aliyepata asilimia 38, alidai kuwa matokeo hayo yalikuwa yamegubikwa na udanganyifu.
Hakufanikiwa kuwasilisha pingamizi la kisheria dhidi ya matokeo hayo kwa kuwa mahakama zilikuwa zimefungwa wiki iliyopita, siku ya mwisho ambayo kesi ingeweza kufunguliwa.
Wachunguzi wa uchaguzi walisema kuwa ingawa siku ya kupiga kura ilikuwa ya amani kwa kiasi kikubwa, baadhi yao waliibua maswali kuhusu mchakato wa kujumlisha kura.
Tunachojua kufikia sasa kuhusu shambulio la Marekani katika harusi huko Sirik Iran?
Saa moja baada ya kuanza kwa mashambulio ya anga ya Marekani dhidi ya maeneo ya kusini mwa Iran ambayo kwa mujibu wa CENTCOM yalilenga vituo na silaha za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, vyombo vya habari nchini Iran viliripoti kuwa sherehe ya harusi katika bandari ya Koh-e-Sirak ililengwa, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua watano, akiwemo mtoto mmoja, na majeraha kwa watu wengine wasiopungua 68.
Vyombo vya habari ndani ya Iran, ikiwemo Shirika la Utangazaji la Iran, vilichapisha picha zilizodaiwa kuwa za eneo la shambulio hilo.
Kuhusiana na hayo, chanzo cha habari cha eneo hilo kililiambia BBC Persian kuwa kinaamini lengo la shambulio hilo la anga lilikuwa "mnara wa mawasiliano" uliopo "mita chache kutoka nyumba iliyofanyika harusi hiyo."
Chanzo hicho cha eneo hilo kililiambia BBC Persian kuwa kwa sasa kuna "uhitaji mkubwa wa michango ya damu" na kwamba barabara zinazoelekea eneo lililoshambuliwa zimefungwa.
Wakati huo huo, Kapteni Tim Hawkins, msemaji wa CENTCOM, alijibu swali kutoka BBC Persian kwa kusema kuwa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) "inafahamu" ripoti zinazohusu tukio hili na kusisitiza kuwa "vikosi vya Marekani havilengi kamwe raia katika mashambulio yao."
Jeshi la Jordan ladai "kuzuia na kuharibu makombora 10 kati ya 13" yaliyofyatuliwa na Iran
Katika taarifa iliyothibitisha shambulio la makombora dhidi ya nchi hiyo usiku wa Jumanne, jeshi la Jordan lilidai kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga iliweza "kuzuia" na kuharibu "makombora 10 kati ya 13 yaliyofyatuliwa kutoka ardhi ya Iran," na kwamba makombora mengine matatu yaliangukia "maeneo ya mbali yasiyo na makazi ya watu."
Saa moja iliyopita, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi kilitangaza mashambulio ya makombora dhidi ya kambi za Marekani nchini Jordan na kutoa picha zinazohusishwa na mashambulio hayo pamoja na mwendo wa makombora angani juu ya Jordan.
Katika taarifa yake, Walinzi wa Mapinduzi walidai kuwa "makombora ya balistiki yalilenga kambi ya Jeshi la Majini la Marekani nchini Jordan, inayojulikana kama Camp Titin, iliyoko kwenye mwambao wa Ghuba ya Aqaba."
Wakati huo huo, jeshi la Kuwait lilitangaza asubuhi ya Jumatano kuwa limewasha mifumo yake ya ulinzi wa anga ili kukabiliana na kile ilichokiita "vitu vinavyorushwa vyenye nia ya uhasama" na kuwataka wananchi kuzingatia maelekezo ya usalama yaliyotolewa.
Trump: Sijaribu kuileta Iran kwenye meza ya mazungumzo
Rais wa Marekani Donald Trump, katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social usiku wa Jumanne, alikanusha ripoti ya ABC News kwamba utawala wake ulikuwa ukijaribu kuilazimisha Iran kufanya mazungumzo, akisema hajali kuhusu kufikia makubaliano na Tehran.
"Kinyume na kile ambacho ABC ambayo (yeye huiita) Habari za Uongo imeiripoti, sijaribu kuileta Iran kwenye meza ya mazungumzo. Sijali hata kidogo kama watatia saini makubaliano ambayo hayana thamani kwao," Bw. Trump aliandika.
"Napendelea zaidi hali ya sasa, ambapo tuna udhibiti karibu kamili wa Mlango-Bahari wa Hormuz na uchumi wa Iran unaporomoka kabisa. Wanachelewesha tu mchakato ambao hauepukiki," aliongeza.
Rais wa Marekani aliandika mwishoni mwa ujumbe huu: "Ni lini watu wa Iran watainuka na kupambana?"
Kauli hizi zilitolewa saa chache baada ya Trump kuelezea mashambulizi mapya ya Marekani dhidi ya maeneo karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz kuwa ya "haki" na kuonya kwamba Washington ingefanya mashambulizi makali zaidi iwapo Iran ingechukua hatua yoyote ya kulipiza kisasi.
Iran inasema mashambulizi hayo yalilenga raia katika sherehe ya harusi katika kijiji cha Kohstak Sirik, na kuua angalau watu watano, akiwemo mtoto mmoja. Vyombo vya habari vya Iran vinaripoti kuwa zaidi ya watu 60 walijeruhiwa katika tukio hilo.
Ujerumani yaishutumu Urusi kwa shambulio la uwanja wake wa ndege Leipzig
Ujerumani imesema Urusi ilihusika na shambulio la ndege zisizo na rubani mwezi uliopita katika uwanja wa ndege wa Leipzig.
Droni iliobeba kilipuzi iligunduliwa katika Uwanja wa ndege wa Leipzig/Halle mashariki mwa Ujerumani, karibu na ndege za mizigo za Ukraine, mnamo tarehe 4 Agosti.
Ilishindwa kulipuka kwani kipuzi hicho kilikuwa na hitilafu, na wachunguzi wanashuku kuwa ndege ya pili isiyo na rubani iligongana na ndege ya mizigo iliyokuwa karibu.
Ndege ya tatu isiyo na rubani iliripotiwa kupatikana karibu na uwanja wa ndege siku 10 baadaye.
Waziri wa mambo ya ndani Alexander Dobrindt alisema shambulio la uwanja wa ndege wa Leipzig lilifuata "mfumo uliowekwa vizuri wa shughuli mseto za Urusi barani Ulaya" na dhana ilikuwa kwamba Ujerumani ingelengwa tena.
Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Jumanne aliishutumu Ujerumani kwa kuweka ushahidi wa kulaumu Moscow kwa jaribio la shambulio la ndege zisizo na rubani katika uwanja wa ndege wa Leipzig.
Putin hakutoa ushahidi wa shutuma hiyo.
Wakati huo huo, ubalozi wa Urusi huko Berlin ulisema madai kwamba Urusi ilihusika yalikuwa "ya kipuuzi".
Dobrindt alisema uchunguzi wa vifaa vilivyotumika pamoja na matokeo ya kijasusi ulithibitisha kuhusika kwa Urusi katika shambulio hilo.
Iran yalipiza kisasi baada ya mashambulizi ya Marekani kuua watu wanne katika harusi
Vikosi vya Marekani vilianza tena mashambulizi dhidi ya Iran siku ya Jumanne, kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom).
Centcom ilisema mashambulizi hayo ya Marekani yalifuatia "jaribio la hivi karibuni la mashambulizi" lililofanywa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) dhidi ya meli za kibiashara katika Mlango-bahari wa Hormuz.
Shirika la Red Crescend la Iran lilisema watu wanne, akiwemo mtoto mdogo, waliuawa na zaidi ya 50 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya Marekani, baada ya vipande vya kombora la Marekani kugonga nyumba ambamo sherehe ya harusi ilikuwa ikiendelea huko Sirik, kusini mwa Iran.
Kama jibu, Iran ilianzisha mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq na Jordan, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya eneo hilo na Jeshi la Jordan. Mashambulizi pia yaliripotiwa Kuwait na Bahrain.
IRGC ilisema Marekani "itajutia" mashambulizi hayo. Kufikia mapema Jumatano, ilikuwa imerusha mfululizo wa makombora ya balistiki kuelekea kambi ya Jeshi la Majini la Marekani (Marines) huko Aqaba, Jordan, ikiwa ni kulipiza kisasi kwa shambulio la Sirik, kulingana na shirika la habari la Iran lisilo rasmi kikamilifu, Tasnim.
Jeshi la Jordan lilisema lilizuia makombora 13 ya balistiki; 10 kati yake yaliangamizwa, huku matatu yakiangukia maeneo ya mbali. Hakukuwa na vifo wala majeraha kutokana na shambulio hilo la Iran.
Mtandao huo pia ulisema kuwa kituo cha usalama wa taifa cha nchi hiyo kilikuwa kimetoa tahadhari kwa wakazi wa mikoa ya Aqaba na Mafraq kuhusu vipande vinavyoanguka kutoka angani, na kuongeza kuwa tahadhari hiyo imeondolewa.
Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja