Kuishi na wazazi 'wahalifu': 'Wazazi wangu walitafutwa na FBI kwa miaka mingi'

Chanzo cha picha, Zayd Ayers Dohrn
"Hata nilipokuwa mdogo sana, walinifundisha masomo ya kimapinduzi… Walinifundisha jinsi ya kuwatambua polisi waliovaa kiraia na maajenti wa FBI ndani ya umati wa watu… Walinifundisha jinsi ya kuwasiliana kwa lugha ya siri kupitia simu… Kwangu, ilionekana kama mchezo."
Zayd Ayers Dohrn hakuwa na utoto wa kawaida.
Hakukuwa na picha za wahusika wa filamu za Disney zilizoning'inizwa kwenye kuta za chumba chake. Badala yake, kuta hizo zilikuwa na picha za Che Guevara na Ho Chi Minh, kana kwamba walikuwa wakimtazama.
Kwa miaka kadhaa, hakuweza kwenda shule ya chekechea. Safari za familia za kupiga kambi hazikuhusu kuchoma pelemende aina ya marshmallow kwenye moto, bali katika tukio moja, zilihusu kuchunguza gereza la serikali kabla ya kutekeleza mpango wa kutorosha mfungwa.
Zayd alipozaliwa, mama yake, Bernadine Dohrn, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakitafutwa zaidi na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
Alikuwa kiongozi wa Weather Underground, kundi lenye msimamo mkali lililopinga vita na lililotaka kuangazia ukosefu wa usawa wa kijamii na dhuluma za rangi nchini Marekani kupitia mfululizo wa milipuko ya mabomu iliyolenga majengo muhimu ya serikali, yakiwemo Bunge la Marekani (Capitol), Pentagon na Idara ya Mambo ya Nje.
Baba yake, Bill Ayers, pia alikuwa mmoja wa waanzilishi wa kundi hilo. Kutokana na hali hiyo, familia hiyo iliishi kwa kutumia majina bandia, ilihama mara kwa mara na ilikuwa daima katika tahadhari dhidi ya kukamatwa.

Chanzo cha picha, Bettmann Archive/Getty Images
Hata hivyo, kwa Zayd, hayo yote yalikuwa maisha yake ya kila siku.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Nilijua FBI ilikuwa ikitufuatilia. Hawakuwahi kunidanganya kuhusu hilo. Walinieleza kwa namna waliyoona mtoto angeweza kuelewa. Kwa mfano, walitulinganisha na Robin Hood. Tulikuwa wahalifu waliowaibia matajiri na kuwapa maskini, mambo ya aina hiyo."
Wazazi wake wote wawili walitoka katika familia za wazungu wa tabaka la kati zilizokuwa na uwezo mzuri wa kiuchumi. Mama yake alikuwa mwanafunzi aliyepata alama za juu katika masomo yake ya sheria katika Chuo Kikuu cha Chicago.
Hata hivyo, baada ya Dkt. Martin Luther King Jr. kufika jijini Chicago na kuunga mkono migomo ya wapangaji iliyofanywa na wanaharakati mwaka 1966, mama yake Zayd alijihusisha kikamilifu na harakati hizo na kuanza kuamini zaidi kwamba Marekani ilihitaji mabadiliko makubwa zaidi.
Kuuawa kwa King, na baadaye kupigwa risasi na kuuawa na polisi kwa Fred Hampton, kiongozi wa chama cha Black Panther, kulimsukuma zaidi kuelekea katika harakati za kutumia nguvu.
"Nadhani tukio hilo lilimfanya mama yangu na watu wengine wachache kama yeye kupoteza kabisa utulivu wa akili," alisema Zayd. "Alimwona Hampton si tu kama rafiki, bali pia kama mtu wa kuigwa, na serikali ikamuua."

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa upande wa baba yake, ni upinzani dhidi ya Vita vya Vietnam na huduma ya kijeshi uliomvuta awali kujiunga na kundi hilo.
"Wakati huo walikuwa na kaulimbiu iliyosema, 'Leteni vita nyumbani.' Wazo lilikuwa kuleta vurugu za Vita vya Vietnam na kuziweka katika mitaa ya Marekani… ili kuwaamsha watu na kuwaonyesha kile walichokuwa wakifanya ng'ambo na kile walichokuwa wakiwafanyia makundi na viongozi weusi hapa nyumbani."
Bomu ndani ya mkoba

Chanzo cha picha, Gado/Getty Images
Wazo kwamba kundi la wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka familia za tabaka la kati lingeweza kufanikiwa kulipua baadhi ya majengo ya serikali yaliyokuwa na ulinzi mkali zaidi nchini linaweza kuonekana la kushangaza.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Zayd, wanachama wa kundi hilo waliweza kutumia dhana zilizokuwepo kuhusu wao kuwa vijana, wazungu na wenye elimu.
Wanawake waliojifanya makatibu waliingia katika majengo hayo kukusanya taarifa na kuweka vilipuzi katika maeneo yaliyokuwa mbali na macho ya watu, mara nyingi ndani ya vyoo vya wanawake.
"Moja ya faida walizokuwa nazo ni kwamba walikuwa na elimu ya juu, waliweza kujieleza vizuri na walikuwa wanaume wazungu wenye uwezo mzuri wa kiuchumi. Wangeweza kupita katika maeneo hayo yenye mamlaka bila kuvutia umakini mkubwa," alieleza Zayd.
Tofauti yao ya rangi pia iliathiri namna walivyoshirikiana na Black Liberation Army, kundi lililojitenga kutoka Chama cha Black Panther.
Wanaharakati hao wazungu walitumia nafasi yao ya kutovutia sana uchunguzi na hadhi yao katika jamii kusaidia wanaharakati weusi, ikiwa ni pamoja na kuwapa usafiri baada ya kutoroka gerezani na kuwasaidia katika shughuli nyingine zilizokuwa kinyume cha sheria.

Chanzo cha picha, Bettmann/Corbis photo via FBI
Kadiri Zayd alivyokuwa akikua, hali halisi ya maisha ya kujificha ilianza kuathiri zaidi utoto wake. Bila nyaraka rasmi, hakuweza kwenda shule, na marafiki zake wengi walikuwa watoto wa wanaharakati wenzake.
Sehemu kubwa ya utoto wake ilifanana na ule wa watoto wengine wa Marekani, ukiwa na safari za barabarani, matembezi ya kifamilia na likizo za kupiga kambi. Hata hivyo, shughuli hizo zilikuwa na sura ya kipekee ya kimapinduzi.
"Hakika hatukuwahi kwenda Disneyland, Bungeni au maeneo kama hayo. Wazazi wangu walinipeleka kutembelea maeneo yaliyohusiana na mapambano ya kimapinduzi… maeneo ambako mashujaa wao waliuawa… ambako polisi walimuua Fred Hampton, ambako John Brown alinyongwa, na ambako Nat Turner aliongoza uasi wa watumwa. Kwa hiyo, ilikuwa kama ziara ya kuzunguka Marekani kama eneo ambalo walikuwa wakipigania mabadiliko."
Ilikuwa miaka mingi baadaye ndipo alipogundua kwamba mojawapo ya safari za familia za kupiga kambi ilikuwa na lengo jingine.
Eneo walilopiga kambi lilikuwa umbali wa chini ya kilomita moja kutoka gereza la serikali ambako mwanachama mmoja wa Black Panther alikuwa amefungwa. Wazazi wake walitumia likizo hiyo kulichunguza gereza hilo kabla ya uwezekano wa kujaribu kumtorosha mfungwa huyo.

Chanzo cha picha, Zayd Ayers Dohrn
Zayd anaamini wazazi wake walikuwa wakijaribu kwa dhati kuepuka kusababisha madhara ya kimwili. Maonyo yalitolewa kabla ya milipuko hiyo, na mabomu yalipangwa kulipuka wakati majengo yalipokuwa matupu.
Hata hivyo, alisema, mara harakati zinapogeukia matumizi ya vurugu, huwa vigumu kuepuka kabisa majanga.
"Wakati mwingine maamuzi yao huwa na hatari, ni ya kuhatarisha maisha na hata yanaweza kuleta matokeo yaliyo kinyume na malengo yao… Wanafanya mambo ambayo yanaweza kuwa mabaya sana na kusababisha majanga makubwa."
Kabla Zayd hajazaliwa, ajali iliyotokea wakati wa kutengeneza bomu ilisababisha kifo cha aliyekuwa mpenzi wa baba yake wakati huo pamoja na wanachama wengine wawili wa kundi hilo.
Hata alipokuwa mtoto, alielewa hatari zilizokuwepo.
"Kwa hakika nilikuwa na wasiwasi kuhusu hilo… Nina marafiki ambao wazazi wao waliuawa. Nina marafiki ambao wazazi wao walifungwa gerezani kwa muda mrefu sana."

Chanzo cha picha, Getty Images
Akiwa mtu mzima, na sasa akiwa baba, Zayd amekuwa akipambana kwa miaka mingi kutafakari maamuzi yaliyofanywa na wazazi wake.
Alilinganisha mtazamo wao na ule wa watu wanaojitolea kujiunga na jeshi. Alisema wanaamini kwamba wanashiriki katika vita dhidi ya serikali yao wenyewe na wako tayari kukubali matokeo ya maamuzi yao.
"Ninajivunia mambo mengi kuhusu wao… Wakati ambapo watu wengi nchini Marekani, hasa wazungu, walikuwa tayari kupuuza dhuluma walizoziona bila kuchukua hatua yoyote, wazazi wangu walikuwa miongoni mwa watu waliokataa kukaa kimya na kusisitiza kwamba lazima wafanye jambo."
Hata hivyo, Zayd anapata ugumu kufikiria mazingira ambayo yeye mwenyewe angeamua kwenda kuiba benki au kumtoa mtu gerezani kwa dhamana huku akiwaacha watoto wake nyumbani.
"Lakini pia nafikiri hilo ni suala la upendeleo wa hali ya maisha. Nafikiri kuna watu wengi duniani ambao hawana chaguo jingine isipokuwa kuhatarisha usalama wa familia zao ili kupambana na ukandamizaji na dhuluma."

Chanzo cha picha, Zayd Ayers Dohrn
Baada ya kuzaliwa kwa mdogo wake Zayd, Bernadine hatimaye aliamua kukubali makubaliano ya kukiri kosa na kujisalimisha kwa mamlaka, ili familia yake iweze kuishi maisha ya kawaida kwa kiasi fulani.
Mwanzoni, aliepuka kufungwa gerezani kutokana na mbinu haramu zilizotumiwa na dosari katika uchunguzi wa FBI. Hata hivyo, baada ya kukataa kutoa ushahidi dhidi ya wanachama wenzake wa Weather Underground, alifungwa gerezani kwa karibu mwaka mmoja.
Baba yake Zayd alibaki na jukumu la kumlea yeye na mdogo wake, pamoja na mtoto wa mwanaharakati mwingine aliyekuwa amefungwa gerezani.
Wakati huo, akiwa na umri wa miaka mitano, Zayd alikuwa na huzuni na hasira, huku akimsihi mama yake arudi nyumbani. Bernadine alimwandikia barua kutoka gerezani akijaribu kumweleza hali ilivyokuwa, na hadi leo bado anazisoma barua hizo.
"Alikuwa akisema kwamba kuwa mama ndilo jambo muhimu zaidi duniani kwake, na kwamba kuwa mwanamapinduzi pia lilikuwa jambo muhimu zaidi duniani kwake," alisema Zayd.
"Alikuwa akimtaja, kwa mfano, mashujaa wake kama Martin Luther King Jr., Fred Hampton na Malcolm X-watu waliopigania jambo fulani - na wote walikuwa na watoto."

Chanzo cha picha, Michael Loccisano/Getty Images
Kwa sasa, wazazi wake wote wawili wako katika miaka ya themanini.
Zayd anawaelezea kama "babu na bibi wazuri sana." Hata hivyo, anacheka anaposikia dhana kwamba uzee umewafanya wapunguze makali ya misimamo yao ya kisiasa.
Baada ya kuacha maisha ya kujificha, mama yake akawa profesa wa sheria na alitumia miongo minne kuendesha kliniki ya kisheria, akiwasaidia watu ambao aliamini walikuwa wameonewa na mfumo wa haki ya jinai usio wa haki.
Baba yake naye akawa profesa na kujitolea katika juhudi za kurekebisha mfumo wa elimu ya umma.
Mbinu zao zinaweza kuwa zimebadilika, lakini imani yao bado ni thabiti.
"Wangeudhika sana ikiwa mtu angewaita watu wenye misimamo ya wastani au waliberali," alisema Zayd.
Makala haya yametokana na kipindi cha Outlook cha BBC World Service, kilichoitwa: "Watu wanaotafutwa zaidi na Marekani: Familia yangu iliyokuwa mafichoni."



































