Kim Jong Un aonekana hadharani tena, kwa nini uvumi wa kifo chake huibuka kila mara?

.
Maelezo ya picha, Vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini vilichapisha picha za Kim Jong Un muda mfupi baada ya uvumi kuhusu kifo chake kuanza kusambaa mtandaoni.
    • Author, Laura Bicker
    • Nafasi, China correspondent
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Kim Jong Un ameonekana kwenye vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini akiwa na afya nzuri kwa kiasi cha kushangaza, licha ya uvumi kwamba amefariki kutokana na kuvuja damu kwenye ubongo.

Picha zilizochapishwa na gazeti la serikali la Rodong Sinmun zinamwonyesha dikteta huyo mwenye umri wa miaka 42 akitembelea maonyesho ya nguo na viatu, ambayo kwa mujibu wa gazeti hilo, aliambatana na binti yake.

Picha hizo zilitolewa saa chache baada ya mpinzani wa serikali ya China anayeishi Marekani kudai, bila kutoa ushahidi, kwamba Kim alikuwa amelazwa hospitalini mjini Beijing akiwa katika hali ya kupoteza fahamu na hatimaye kufariki dunia.

Kwa watu wanaofuatilia kwa karibu masuala ya Korea Kaskazini, uvumi wa aina hii umekuwa jambo la kawaida.

Katika moja ya mataifa yaliyoficha zaidi taarifa zake duniani, mara nyingi ni vigumu kuthibitisha ukweli, hali inayotoa nafasi kubwa kwa dhana na uvumi.

Dai hili la hivi karibuni lilitolewa na Wanjun Xie, ambaye anajitambulisha kuwa mwenyekiti wa Chama cha Kidemokrasia cha China, kikundi kilichopigwa marufuku na mamlaka za China. Hapo awali, amewahi kusambaza madai ambayo hayajathibitishwa, yakiwemo uvumi kuhusu kifo cha kiongozi wa China, Xi Jinping.

Xie alidai kuwa Kim alipata tatizo kubwa la kuvuja damu kwenye ubongo na kuhamishiwa Beijing kwa sababu Korea Kaskazini haina vifaa vya kutosha vya kitabibu kumtibu.

Alidai kuwa Kim alifariki baadaye na mwili wake kurejeshwa kwa siri nchini Korea Kaskazini, huku serikali ikificha taarifa za kifo chake.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, picha hizo zinaonesha hali tofauti.

Kim anaonekana akikagua bidhaa zilizooneshwa kwenye maonyesho hayo, akiwa ameambatana na Kim Ju Ae pamoja na kundi la maafisa wanaoandamana naye mara kwa mara.

Ingawa hakuna njia ya kujua kwa uhakika ni lini picha hizo zilipigwa, kuna sababu nyingine zinazofanya dai hilo kutiliwa shaka.

Huenda kungekuwa na dalili nje ya mipaka ya Korea Kaskazini iwapo afya ya Kim ingezorota ghafla.

China ingeweza kuimarisha ulinzi katika mpaka wake ili kujiandaa na uwezekano wa machafuko au wimbi la wakimbizi. Shughuli katika ofisi za kidiplomasia za Korea Kaskazini pia zingeweza kuongezeka. Wakimbizi waliotoroka Korea Kaskazini na kuishi Korea Kusini mara nyingi hupata taarifa kupitia mitandao isiyo rasmi iliyo kando ya mpaka wa China. Hakuna dalili yoyote kati ya hizo iliyojitokeza.

Wakati huohuo, maafisa wa kijasusi wa Korea Kusini waliiambia shirika la habari la Yonhap kwamba hawakuwa na taarifa zozote zinazounga mkono madai hayo.

Uvumi huo pia unafanana na madai ya uongo yaliyowahi kutolewa hapo awali.

Mwaka 2020, mkimbizi maarufu kutoka Korea Kaskazini alidai kuwa alikuwa na uhakika wa asilimia 99 kwamba Kim alikuwa amefariki baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu. Muda mfupi baadaye, Kim alionekana hadharani na hivyo kufichua udhaifu wa dai hilo.

Kwa hiyo, kwa nini uvumi huu unaendelea kujitokeza?

Sababu ya kwanza ni suala la urithi wa uongozi

Korea Kaskazini imekuwa ikitawaliwa na familia ya Kim kwa vizazi vitatu, lakini kile kitakachotokea baada ya Kim Jong Un bado hakina uhakika kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.

Kim Il Sung alitumia miongo kadhaa kumwandaa mwanawe, Kim Jong Il, kushika madaraka. Kufikia wakati Kim Il Sung alipofariki mwaka 1994, mpango wa kumrithi ulikuwa umeandaliwa vizuri. Mabadiliko ya uongozi kutoka kwa baba kwenda kwa mwanawe yalifanyika kwa utulivu wa kiasi.

Kupanda kwa Kim Jong Un madarakani kulikuwa kwa haraka zaidi na kulikabiliwa na changamoto nyingi. Baada ya Kim Jong Il kupata kiharusi mwaka 2008, mwanawe mdogo zaidi alipandishwa vyeo haraka ndani ya mfumo wa uongozi. Kufikia wakati baba yake alipofariki mwaka 2011, tayari alikuwa ametajwa hadharani kuwa kiongozi mtarajiwa.

Hata hivyo, Kim Jong Un alitumia miaka kadhaa kuimarisha mamlaka yake, kuwaondoa wapinzani katika nyadhifa zao na kuangamiza watu aliowaona kuwa vitisho.

Kwa sasa, shirika la kijasusi la Korea Kusini linaamini kwamba huenda anamuandaa binti yake kuwa mrithi wake. Binti huyo amekuwa akionekana zaidi katika matukio muhimu ya kitaifa na maonesho ya kijeshi.

Hata hivyo, anadhaniwa kuwa na umri wa miaka 13 pekee. Korea Kaskazini haijawahi kuongozwa na mwanamke, na binti huyo bado hajatangazwa rasmi kuwa mrithi wa uongozi. Umri wake mdogo pia unaweza kumfanya awe katika hatari ya kukabiliwa na mapambano ya kuwania madaraka.

Kutokuwa na uhakika huku kunasaidia kueleza kwa nini uvumi kuhusu afya ya Kim huvutia watu wengi.

.
Maelezo ya picha, Idara ya ujasusi ya Korea Kusini inaamini kuwa huenda Kim Jong Un anamuandaa binti yake kuwa mrithi wake.

Sababu ya pili ni kwamba uvumi huo hauko mbali kabisa na uwezekano wa kutokea

Kim ana uzito mkubwa wa mwili na anavuta sigara kwa wingi. Shirika la Kijasusi la Korea Kusini limekuwa likionya mara kadhaa kwamba mtindo wake wa maisha unamuweka katika hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu. Matatizo ya moyo na kiharusi pia yamewahi kutokea katika familia ya Kim.

Iwapo jambo lolote lingemtokea Kim, athari zake zingekuwa kubwa kwa nchi jirani na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla.

Mgogoro wowote wa ghafla wa uongozi ungeibua maswali magumu kuhusu udhibiti wa silaha za nyuklia za Korea Kaskazini na uwezekano wa kutokea kwa machafuko ya kisiasa.

Je, mapambano ya kuwania madaraka yangewashawishi viongozi wenye misimamo mikali kuchukua hatua za uchokozi? Je, machafuko yangesababisha mgogoro wa wakimbizi katika mpaka wa China?

Haya ni maswali yanayozitia wasiwasi si Beijing na Seoul pekee, bali pia Washington, ambayo ina takribani wanajeshi 28,000 nchini Korea Kusini.

Mashirika ya kijasusi yanafuatilia kwa karibu mwenendo wa Kim Jong Un ili yawe tayari kukabiliana na taarifa zozote zinazoweza kujitokeza.

Kwa kuwa Korea Kaskazini bado ni nchi ambayo taarifa zake ni ngumu sana kupatikana na kuthibitishwa, pia imekuwa rahisi kwa taarifa za uongo kusambaa kuihusu.

Ni watu wachache sana wanaoweza kukutana na kiongozi huyo mara kwa mara. Hata mashirika ya kijasusi yanapata ugumu wa kupata taarifa za kuaminika, na taarifa nyingi zinazopatikana huambatana na tahadhari kwamba hazijathibitishwa au kuna uwezekano mkubwa wa kuwa za kweli, badala ya kuthibitishwa kikamilifu.

Pia, serikali ya Korea Kaskazini inashukiwa kuchochea kwa makusudi hali ya mkanganyiko kwa kusambaza taarifa zinazopotosha ili kuficha kinachoendelea ndani ya nchi hiyo.

Kwa hiyo, ni vigumu kuamini kwamba Wanjun Xie alipata kwa bahati taarifa muhimu kiasi hicho, wakati ambapo taarifa hiyo haikuwa imefahamika kwa wale ambao kazi yao ni kufuatilia kwa karibu mwenendo wa Korea Kaskazini.

Huenda alikuwa akitafuta tu kuvutia umakini wa watu. Au huenda alitaka kuiaibisha Beijing kwa kuangazia uhusiano wake na Pyongyang, ingawa uhusiano huo unajulikana wazi duniani.

Bila kujali nia yake, Xie si mtu wa kwanza kutumia hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu uongozi wa Korea Kaskazini kwa manufaa yake.