Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
WARIDI WA BBC: 'Ulishawahi kumuona bilionea Mo Dewji akifunza watu elimu ya fedha'?
- Author, Martha
- Nafasi, BBC SWAHILI
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mimi ni zao la talaka. Kama ningebaki nyumbani nisingesoma kutokana na uwezo mdogo kiuchumi aliokuwa nao baba yangu ambaye nilibaki nae baada ya kuachana na mama.
Ndivyo anavyoanza kusimulia Lilian Simpson Mwalimu wa chuo cha usimamizi wa fedha nchini Tanzania aliyejipatia wafuasi mtandaoni kwa kutoa elimu ya fedha na uwekezaji mtandaoni.
Akiwa na umri wa miaka 16 tu, aliondoka nyumbani kwao akitafuta mazingira bora ya kusoma. Shule ikiwa mbali na nyumbani, alipata hifadhi kwa rafiki yake, aliyeishi na mama yake pekee.
'Ninakumbuka kupambana na usafiri au kutembea kwa miguu kutoka nyumbani Kivule hadi shuleni Buguruni umbali huo ulinichosha' alisema Lilian
Kiu yangu kupata elimu ilinisukuma kuvumilia changamoto nyingi nilizopitia wakati wote wa elimu ya sekondari hasa baada ya wazazi wangu kutalikiana.
Baba yangu ambaye alikuwa mchungaji aliridhia nikajitafute ili kutimiza ndoto yangu ya kupata elimu.
Nilifanya vizuri mitihani yangu ya sekondari na kujiunga na chuo kikuu cha usimamizi wa fedha IFM.
Lilian ambaye alifanya vizuri katika mitihani yake ya sekondari na chuo anasema muda wote akiwa shuleni na hata chuoni alipenda kuwakusanya wenzake na kuwashawishi kucheza 'upatu' na kuwa kiongozi wao kwa kukusanya fedha na kumpatia muhusika mwisho wa mwezi,na kila mwanakikundi alipaswa kumlipa kiasi kidogo kwa kuwasimamia mchezo huo wa kupeana pesa.
'Walinilipa kwa sababu mimi niliwafahamu wote na kuwakutanisha kucheza mchezo huo'
Hivyo ndivyo nilivyoweza kukusanya kipato kidogo kidogo.
Sikuwa na maisha ya anasa chuoni. Sikujihusisha na mambo yoyote ambayo yangenitumbukiza viwashawishini au kurudisha nyuma ndoto zangu.
'Kuishi nje ya kipato ni makosa yanayofanywa kwa kujua au kutokujua'
Kitaaluma Lilian anasema yeye ni mwalimu lakini linapokuja suala la fedha na uwekezaji anajiona kuwa ushuhuda unaotembea.
Hii ni kutokana na kwamba anachokifundisha ni halisi na dhahiri katika maisha yake.
'Ninafahamu kuishi maisha magumu, kuiheshimu kila senti ninayoipata kwa malengo ya kuizalisha zaidi'.
Nilianza kufanya biashara ya vipodozi nikiwa chuo,ilinisaidia kupata pesa ya kujikimu kidogo na kumsaidia baba yangu pia.
Mimi nilikuwa na ndoto niliyotaka kuitimiza. Kuwa na kipato changu na hata kuweza kurithisha uzao wangu utajiri nitakaojitengenezea baadae kutokana na shughuli nitakazoendelea kufanya.
Lilian anasisitiza kwamba katika mikutano yake na wasichana au wanawake amekuwa akisisitiza kila mmoja kuwa na ndoto ya miaka 5 au hata 10 ijayo.
Unafanya nini kutimiza hayo malengo? nimepata uzoefu kutoka kwa vijana wengi ninaokutana nao hujikuta wakifanya makosa ya kifedha mara baada y akuanza kupata kipato kutokana na kukosa kuwa na elimu ya fedha.
Ukishajua huna elimu ya fedha inakupasa uitafute,kwa msaada wa mitandao unaweza kujifunza walau kwa kiwango cha kuweka akiba na kuwa na bajeti.
Kuishi nje ya kipato ni moja kati ya makosa ambayo baadhi ya watu wanafanya kwa kujua au kwa kutojua.
'Wewe ni mwanamke, masikini, utanifundisha nini ?
Baadhi ya watu kwenye jamii bado hawana imani na uwezo wa wanawake katika kutoa elimu ya fedha na uwekezaji.
Kitu cha kwanza niliambiwa hivi ulishawahi kumuona Mo Dewji akifundisha watu elimu ya fedha?
Ni nyie masikini ndio mnafundisha watu kuhusu fedha..anaendelea kusimulia kuwa wakati mwingine aliambiwa 'We ni mdogo tuambie kuna mwanaume gani nyuma anayekufadhili'
"Kwahiyo tunataka MO ndo aje asimame atuambie fanya hivi fanya hivi, wewe ni maskini mwenzangu"
"Kwahiyo hiyo ndio changamoto ninayokutana nayo wewe ni mwanamke, wewe ni maskini, hauna hiki wala hiki utanifundisha nini wakati hauna kitu?"
Mathalan kuna watu wanaothamini na kupokea elimu ninayoitoa na hata kunitafuta kuwafundisha na wananilipa.
'Mitandao ya kijamii inatufungulia fursa sisi ambao hatuna 'connection'
Lilian anasema watu wanatafuta watu wa kujihusianisha nao.
Unaona ile 'stori' yangu mtandaoni kuwa nilitoka nyumbani nikiwa na miaka 16 iliniletea wasichana wengi 'DM' wenye uzoefu kama wangu.
'Wapo waliotoka nyumbani kwa kutoroka au kuondoka tu kwa ridhaa za wazazi wakajitafute na walikutana na vikwazo vingi vilivyokwamisha ndoto zao na kuwafanya wakate tamaa'
Nimekutana na mabinti walioondoka kwao wakiwa na umri wa miaka 14 na hata 16 kama mimi.
Lilian anatumia fursa hiyo kuwapa matumaini na imani kuwa inawezekana kufanikiwa ukiamua kwani hawako peke yao.
Lilian anasema mitandao ya kijamii imemfanya awe nanga rejea kwa wanawake na vijana anaokutana nao anafundisha kujishughulisha kwa mbinu mbalimbali halali huku wakijiwekea malengo ya kutimiza katika maisha yao.
Kuna wakati Lilian anawaza ingekuwaje kama angetumia mitandao yake kuwatusi na kuwanyanyasa watu?nasi angemsikiliza?
Anafurahi kwamba mitandao imempa fursa ya kutambulika kwenye jamii ya Tanzania, kuitwa na taasisi za kidini ili kutoa elimu ya fedha kwa wanawake ni moja kati ya hatua kubwa kwake.
Wakati mwingine nimekuwa nikifuatwa na vikundi vya wanawake na wanaume kuwapa elimu na wananipatia kiasi fulani cha pesa ,lakini lengo langu kutoa elimu hii mtandaoni mwanzo haikuwa kujipatia kipato.
Ninafurahi kuwasimamia kiuchumi mamia ya wanawake na wanaume kupitia makundi sogozi ya WhatsApp ambapo huwakusanya na kuwapa changamoto na malengo ya kujiwajibisha kuweka akiba, kuelimishana kuhusu elimu ya hisa, uwekezaji wa mifuko ya pamoja na maandalizi ya kustaafu.
Kupitia mitandao ya kijamii nimeweza kujiongezea malengo ya kuwafikia zaidi vijana na wanawake ili kuhakikisha wanaelewa masuala ya fedha.