Kwa nini uchaguzi huu unaweza kubadili siasa za Israel na hatma ya Netanyahu?

Two men wearing suits look ahead. It is Gadi Eisenkot and Benjamin Netanyahu in a composite image.
Maelezo ya picha, Kura za maoni zilizochapishwa Ijumaa zinaonyesha kuwa Gadi Eisenkot (kushoto) na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu (kulia) wanachuana vikali katika kinyang'anyiro hicho.
    • Author, Tom Bennett
    • Akiripoti kutoka, Jerusalem
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Waisrael wanapiga kura katika uchaguzi ambao wengi wanauona kuwa miongoni mwa chaguzi muhimu zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Kura za maoni zilizochapishwa Ijumaa iliyopita zinaonyesha kuwa Waziri Mkuu wa sasa, Benjamin Netanyahu, anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Gadi Eisenkot, mkuu wa zamani wa jeshi, katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya waziri mkuu.

Hata hivyo, hakuna kambi kati ya hizo mbili inayotarajiwa kupata viti 61 vinavyohitajika ili kuunda serikali yenye wingi wa wabunge. Hali hiyo inaashiria uwezekano wa mazungumzo ya kisiasa kuchukua wiki kadhaa au hata miezi kabla ya serikali mpya kuundwa.

Kampeni za uchaguzi zimejikita zaidi katika suala la usalama. Kambi ya upinzani imemkosoa Netanyahu kutokana na kile inachokiita kushindwa kwa kiwango kikubwa kwa mifumo ya usalama ya Israel, kulikowezesha mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas tarehe 7 Oktoba.

Katika mashambulizi hayo, karibu watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka na kupelekwa Ukanda wa Gaza.

Upinzani umetaka kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi kuhusu mashambulizi hayo, jambo ambalo Netanyahu amekuwa akilipinga kwa muda mrefu, akisema tume hiyo haitakuwa na upendeleo na inaweza kumlenga yeye kisiasa.

Licha ya ukosoaji huo, Netanyahu amejitambulisha tena kama kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kulinda usalama wa Israel. Ameelekeza kampeni yake katika kile anachokitaja kuwa ushindi wa kimkakati katika vita vya Israel kote Mashariki ya Kati, pamoja na uhusiano wake wa karibu na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Mfumo wa uchaguzi wa uwakilishi wa uwiano wa Israel unamaanisha kuwa serikali huundwa kupitia muungano wa vyama kadhaa. Hali hiyo imekuwa ikisababisha miungano isiyotarajiwa katika harakati za kuunda serikali.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, uchaguzi huu unaonekana kuwa na ushindani mkali zaidi, huku baadhi ya vyama vikishaanza kuweka wazi masharti ambayo haviko tayari kuyavunja katika mazungumzo ya kuunda serikali.

Eisenkot, anayeongoza chama kipya cha Yashar, ndiye mhusika mkuu katika kile kinachojulikana kama kambi ya mabadiliko. Kambi hiyo inajumuisha vyama vyenye misimamo tofauti ya kiitikadi, lakini vinavyounganishwa na lengo la kumuondoa Netanyahu madarakani.

Miongoni mwa viongozi wengine wa kambi hiyo ni aliyekuwa waziri mkuu Naftali Bennett na Avigdor Lieberman, ambao wote wana misimamo ya mrengo wa kulia na misimamo mikali kuhusu usalama. Pia yumo Yair Golan, jenerali wa zamani mwenye misimamo ya mrengo wa kushoto.

Kwa upande wa Netanyahu, mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa ambaye alihudumu kwa mara ya kwanza kama waziri mkuu mwaka 1996, kurejea madarakani kutategemea uwezo wake wa kuunda tena muungano na vyama vya mrengo mkali wa kulia pamoja na vyama vya Wayahudi wa Kiorthodoksi kali vinavyounda serikali yake ya sasa.

Muungano huo unaunda serikali ambayo imeelezwa kuwa yenye misimamo ya mrengo wa kulia zaidi katika historia ya Israel.

Pia kuna miungano miwili ya vyama vya Waarabu inayoshiriki uchaguzi huo. Waarabu wanaunda takriban asilimia 20 ya wakazi wa Israel, wengi wao wakijitambulisha kama Wapalestina wenye uraia wa Israel.

Kinadharia, vyama hivyo vinaweza kuwa na ushawishi mkubwa katika kuamua ni nani atakayeunda serikali. Hata hivyo, karibu vyama vyote vikuu vya Kiyahudi, isipokuwa kimoja, vimekataa kushirikiana navyo.

Mawaziri wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia, Itamar Ben Gvir (kushoto) na Bezalel Smotrich (katikati), wamekuwa miongoni mwa sauti zenye ushawishi mkubwa katika serikali ya Netanyahu. Wanaongoza vyama tofauti vya mrengo huo.

Three men in suits and two women stand speaking to the media in dappled evening sunlight.
Maelezo ya picha, Mawaziri wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia, Itamar Ben Gvir (kushoto) na Bezalel Smotrich (katikati), wamekuwa sauti muhimu ndani ya serikali ya Netanyahu, huku kila mmoja akiongoza chama chake cha mrengo mkali wa kulia.

Demokrasia, kesi ya ufisadi na mageuzi ya mahakama

Kambi ya upinzani pia inasema kuwa kuna wasiwasi kuhusu mustakabali wa demokrasia chini ya uongozi wa Netanyahu.

Netanyahu anakabiliwa na kesi inayoendelea mahakamani kuhusu tuhuma za ufisadi, ambazo anazikanusha. Pia anaendelea kusukuma mbele mipango yenye utata ya kufanya mageuzi katika mfumo wa mahakama, ambayo hapo awali ilisababisha maandamano makubwa nchini Israel kabla ya mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba.

Siku ya Jumapili, kituo cha televisheni cha Israel, Channel 12, kiliripoti kuwa Netanyahu alishinikiza kuchukuliwa kwa hatua za kijeshi katika dakika za mwisho za kampeni, ambazo zingeweza kusababisha makabiliano na Iran kabla ya uchaguzi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mkuu wa jeshi la Israel, Eyal Zamir, alipinga hatua hiyo.

Siku iliyofuata, CNN iliripoti kuwa Netanyahu pia alijaribu kumshawishi Trump kuidhinisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran, lakini Trump alikataa kutoa idhini hiyo.

Netanyahu amekanusha ripoti zote mbili.

Pia alizua mjadala katika siku za mwisho za kampeni baada ya kuchapisha picha iliyotengenezwa kwa kutumia akili mnemba (AI), ikionyesha bomu la nyuklia likilipuka mjini Tel Aviv.

Katika ujumbe huo, alionya kuwa yeye ndiye kiongozi pekee anayeweza kuilinda Israel iwapo Iran itapata silaha za nyuklia.

Eisenkot alimjibu kwa kumwita Netanyahu "anayepandisha taharuki kupita kiasi".

Hundreds or thousands of ultra-Orthodox jews stand beside barbed wire fencing.
Maelezo ya picha, Netanyahu kwa sasa yuko katika muungano wa serikali na vyama viwili vya Kiyahudi vya mrengo wa Ultra-Orthodox, ambavyo vimeunga mkono maandamano ya kupinga sheria ya kuwataka wanaume wa jamii hiyo kujiunga na jeshi.

Mgawanyiko kuhusu kujiunga na jeshi

Suala jingine lililotawala kampeni ni ulazima wa kujiunga na jeshi.

Serikali ya Netanyahu imeshindwa kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya Juu unaotaka wanaume Wayahudi wa Kiorthodoksi wenye msimamo mkali wanaojishughulisha na masomo ya dini wakati wote kujiunga na jeshi.

Suala hilo limezua mgawanyiko mkubwa, hasa wakati maelfu ya Waisraeli wengine wamekuwa wakihitajika kujiunga na jeshi na kushiriki katika vita vya hivi karibuni.

Netanyahu kwa sasa anashirikiana na vyama viwili vya Kiorthodoksi vyenye msimamo mkali, ambavyo vimeunga mkono maandamano dhidi ya ulazima wa kundi hilo kujiunga na jeshi.

Msimamo wa Eisenkot kuhusu Gaza na Wapalestina

Eisenkot ana msimamo unaofanana kwa kiasi kikubwa na wa Netanyahu kuhusu Gaza. Ameahidi kukomesha utawala wa Hamas katika eneo hilo ndani ya miezi 18, kupitia mpango wa amani unaoongozwa na Marekani au, ikiwa hilo halitawezekana, kwa kutumia nguvu za kijeshi.

Israel imeendelea kufanya mashambulizi dhidi ya Gaza karibu kila siku tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalipofikiwa mwaka uliopita. Israel inasema mashambulizi hayo yanalenga wanachama wa Hamas.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, ambayo iko chini ya utawala wa Hamas, zaidi ya watu 74,000 wameuawa na jeshi la Israel tangu kuanza kwa vita hivyo. Takwimu hizo zimekuwa zikichukuliwa kuwa za kuaminika na Umoja wa Mataifa.

Israel imekabiliwa na lawama zinazoongezeka kutoka jumuiya ya kimataifa kutokana na mwenendo wake katika vita hivyo, huku uhusiano wake na baadhi ya washirika duniani ukizorota.

Kuhusu Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Eisenkot anaunga mkono kwa kiasi kikubwa makazi ya Israel katika eneo hilo. Makazi hayo yanachukuliwa kuwa kinyume cha sheria za kimataifa.

Hata hivyo, anataka hatua kali zichukuliwe dhidi ya walowezi wa Kiyahudi wenye misimamo mikali wanaowashambulia Wapalestina. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, mashambulizi hayo yamefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa.

Eisenkot pia amezungumzia uwezekano wa kuunda mazingira yatakayowapa Wapalestina uhuru wa kujitawala au kuanzisha taifa lenye mamlaka yenye mipaka, huku Israel ikiendelea kuwa na udhibiti wa mwisho wa usalama.

Wazo la suluhisho la mataifa mawili, linalopendekeza kuundwa kwa taifa huru la Palestina litakaloishi kwa amani sambamba na Israel, limekaribia kutoweka katika mijadala mikuu ya kisiasa nchini Israel.

Baadhi ya wachambuzi wamependekeza kuwa vyama vya Waarabu vinaweza kuunga mkono serikali ya wachache inayoongozwa na Eisenkot bila kujiunga rasmi nayo. Hata hivyo, Lieberman, ambaye ni mmoja wa viongozi muhimu wanaoweza kujiunga na muungano huo, amekataa uwezekano wa kushiriki katika mpango wa aina hiyo.

Misimamo hiyo inaifanya hesabu ya kisiasa ya kuunda serikali kuwa ngumu. Bado haijulikani ni makubaliano gani yatafikiwa, ni masharti gani yatakayolegezwa na ni misimamo gani ambayo vyama vinaweza kubadili baada ya matokeo kutangazwa.

Uchaguzi wenye ushindani mkali

Inaripotiwa kuwa Waisraeli wapatao 70,000 wamesafiri kwa ndege kurejea nchini kutoka nje ya nchi ili kupiga kura, huku takriban nusu milioni wakitarajiwa kushiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza.

Saa 22:00 kwa saa za Israel (20:00 GMT) siku ya Jumanne, vituo vya televisheni nchini humo vitatangaza matokeo ya awali ya kura za maoni zilizofanywa baada ya wapiga kura kutoka vituoni.

Matokeo hayo yatatoa dalili ya mwelekeo wa uchaguzi, ingawa wakati mwingine yanaweza kutofautiana kwa kiasi kikubwa na matokeo rasmi.

Katika maeneo mbalimbali nchini Israel, wafuasi wa vyama watakusanyika kufuatilia matokeo yanavyoanza kutangazwa. Chama cha Likud cha Netanyahu kitakusanyika mjini Jerusalem, huku chama cha Yashar cha Eisenkot, kilichoanzishwa mwaka uliopita pekee, kikikutana mjini Tel Aviv.

Mamia ya maelfu ya wanajeshi na askari wa akiba wa Israel pia watapiga kura. Hata hivyo, kura nyingi za kundi hilo hazitaanza kuhesabiwa hadi Jumatano, jambo linaloweza kuathiri matokeo ya mwisho, hasa kwa vyama vya mrengo wa kulia vinavyoaminika kuwa na uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wanajeshi hao.

Ingawa uchaguzi huu mara nyingi unaelezwa kuwa mashindano kati ya Eisenkot na Netanyahu, bado kuna uwezekano wa kiongozi mwingine kuwa waziri mkuu iwapo ataweza kushawishi chama chake kuunga mkono muungano wa serikali kwa sharti la yeye kupewa nafasi hiyo.

Mojawapo ya hali zinazotia wasiwasi ni uwezekano wa mkwamo wa kisiasa, ambapo hakuna kambi itakayoweza kupata viti vya kutosha kuunda serikali yenye wingi wa wabunge, wala kuunda serikali ya wachache.

Katika hali hiyo, uchaguzi mwingine unaweza kuitishwa, huku Netanyahu akiendelea kuwa waziri mkuu wa mpito.

Kati ya mwaka 2019 na 2022, Israel ilifanya chaguzi tano tofauti huku vyama vikishindwa mara kwa mara kufikia makubaliano ya kushirikiana kuunda serikali.